Ibada Ya Kanisa La Kristo

Yesu alisema, “Lakini saa inakuja, nayo saa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika Roho na Kweli.  Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.  Mungu ni Roho nao wamwabuduo Yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na Kweli,” Yn. 4:23, 24.  Vitu viwili vinahitajika kwa kumwabudu kama tunataka ibada zetu zikubaliwe na Mungu.

  1. Ni lazima tuabudu katika roho.

Hiyo maana yake mioyo yetu lazima iwe katika hali ya haki.  Ni lazima tuwe tunafikiria tukifanyacho. Isa. 1:11-20; Mith. 28:9; Mt. 15:8.

Ni lazima tumwabudu Mungu katika kweli. Kumwabudu Mungu katika kweli maana yake ni lazima kumwabudu Mungu kulingana (kufuatana) na kweli. Neno la Mungu ndiyo kweli (Yn. 17:17).  Kwa hiyo, ili kuabudu kwetu kukubaliwe na Mungu, lazima kufanyike kwa kufuata neno lake.

Agano Jipya linatoa matendo ya ibada ambayo wakristo wanapaswa kuyafanya.  Matendo ya ibada yaliyotolewa katika Agano la Kale kama kucheza, vyombo vya kufukiza uvumba, iliamriwa kwa taifa la Israeli tu.  Agano la Kale kama sheria inayofunga kwa watu wa Mungu iliishia msalabani (Kol. 2:13, 14).  Wakristo ni lazima wajifunze kutoka katika Agano Jipya, sheria ya Kristo kwa watu wote leo, jinsi Mungu anavyotaka aabudiwe leo.  Matendo ya ibada yanayotakiwa na Mungu yameelezwa na kuwekwa wazi ndani ya Agano Jipya.

Chakula cha Bwana:

Chakula cha Bwana au ushirika (1 Kor. 10:16), kinajumuisha vitu viwili (1) mkate usiotiwa chachu (bila chachu) na (2) uzao wa mzabibu (maji ya zabibu).  Kusudi la Chakula cha Bwana ni kuleta kumbukumbu ya dhabihu ya mwili na damu ya Yesu msalabani (Mt. 26:26-29).  Ni lazima tuwe waangalifu tunaposhiriki ushirika huo kuona kuwa tunapambanua ipasavyo na kutambua damu na mwili wa Yesu ili kushiriki katika tabia inayostahili (1 Kor. 11:23-30).  Wakristo ni wajibu wale Chakula cha Bwana kila Siku ya Kwanza ya kila juma (Mdo. 20:7).

Sala (Maombi):

Maombi yanayotolewa kwa Mungu yanapaswa yawe sehemu ya ibada ya jumla (au hadhara) na pia ile ya faragha au pekee.  Kuna mifano mingi ihusuyo mwongozo wa mambo ya sala katika Agano Jipya (1 Tim. 2:1, 2, 8); (Flp. 4:6) n.k.  Katika sala zetu kwa Mungu tunatoa shukurani zetu na kulitukuza jina lake.  Katka sala zetu tunaweza kuomba kwa ajili ya mahitaji yetu na ya wengine.

Yesu alituonyesha “kielelezo”  cha maombi katika Mt. 6:5-15.  Hakukusudia tuwe tunairudia kama wimbo usio na maana katika mawazo lakini aliitoa kama mfano ili kuona jinsi tunavyoweza kuweka maombi yetu.  Yesu Kristo ni Mpatanishi wetu na Kuhani Mkuu.  Kwa hiyo sala zetu ni lazima zielekezwe kwa Mungu kwa njia ya jina la Yesu (Yn. 16:23; 1 Tim. 2:5; Ebr. 4:14-16; 1 Yoh. 2:1, 2).

Kuhubiri na Kufundisha Neno la Mungu:

Mungu ametuamuru kufundisha neno lake (Mt. 28:19,20).  Wote waliookolewa na wenye dhambi wanahitaji kufundishwa.  Kwa hiyo, somo toka ndani ya BIBLIA NI moja ya matendo ya ibada ambayo kwayo wakristo wanapaswa kujishughulisha (Mdo. 2:42).  Ni lazima tujifunze Neno la Mungu ili tuweze kuimarika katika Kristo, kuwafundisha wengine na kuzuia mafundisho mapotofu (1 Pet. 2:1, 2; 2 Tim. 2:2; 4:1-5).  Hii ni sehemu muhimu sana ya ibada yetu na kamwe tusiipuuze.

Kutoa:

Kutoa katika tulivyonavyo ni sehemu ya ibada kwa Mungu.  Hii ni njia inayolifanya Kanisa la Kristo lipate fedha ya lazima kufanyia kazi yake.  Mungu ametupatia mpango mkalilifu unaohusu kutoa (1 Kor. 16:2).  Tumeambiwa ni nani atoe.  “Kila mtu kwenu” tumeambiwa lini tutoe, “Siku ya Kwanza ya juma”  tumeambiwa tutoe kiasi gani, “Kwa kadiri ya kufanikiwa kwetu.”  Tunaonyesha upendo wetu kwa Mungu tutoapo kwa furaha na hiari kwake, 2 Kor. 9:7.

Kuimba:

Wakristo tumeambiwa (tumeamriwa) kumtukuza Mungu katika nyimbo (Kol. 3:16)  aina ya muziki ambao Mungu ameamuru kwa ajili ya Kanisa lake ni wa mdomo tu.  Huo ni kuimba.  Hakuna mahali po pote penye amri au mfano katika Agano Jipya kuhusu kutumia vyombo vya muziki katika ibada ya kikristo.  Kuongeza vyombo vya muziki katika kuimba kwetu ni dhambi.

Kwa sababu ya kuongeza juu ya lile ambalo mungu ametuambia analihitaji (analolitaka) hakuna mtu mwenye haki kufanya hilo (Ufu. 22:18.19; 2 Yoh. 9-11).  Tunatakiwa “kushangilia ndani ya mioyo yetu” (Efe. 5:19) vyombo viwe ni vile vilivyofanywa na Mungu (mdomo) na sio watu!

Wala Mungu hajatuamuru kuwa na waimbaji maalum katika ibada yetu kama wanakwaya; kila Mkristo ni lazima amtukuze Mungu katika wimbo kama vile kila mmoja anavyoshiriki Chakula cha Bwana yeye mwenyewe.  Lengo la kumwabudu Mungu sio kujitumbuiza sisi kwa sisi.  Kwa hiyo, tufanyacho katika ibada siyo kile kinachovutia viungo vyetu vya ufahamu, bali lazima kiwe ni kile kimpendezacho Mungu.

Wakristo wa kweli wanataka kumwabudu Mungu.  Kwa kweli haiwezekani kwa Mkristo wa kweli kutomwabudu Mungu.  Tunapofahamu ukuu wa Mungu, utukufu wake, enzi yake, hekima yake na nguvu na kutafakari juu ya rehema zake zisizopimika (katika ukubwa wake) katika kumtoa mwanawe pekee ili atuokoe kutoka dhambini mwetu, mioyo yetu itafurika “matoleo (dhabihu) ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake,” (Ebr. 13:15)

Na Rod Rutherford

http://www.kanisalakristo.com

 

 

ALA ZA MUZIKI KATIKA IBADA

ALA ZA MUZIKI KATIKA IBADA
Na James M. Tolle (Mtafsiri Chris Mwakabanje)

Utangulizi:

1. Watu wengi wanapotembelea ibada za kanisa la Kristo kwa mara ya kwanza hustaajabia kitendo cha kutokuona ala za muziki ibadani.

2. Tunapaswa kuwa na majibu sahihi (1 Pet.3:15) kuhusu hili kama ilivyo katika mada mbalimbali zinazohusu Biblia.
a. Wasije wakadhani hatupendi tu kutumia vyombo vya muziki, au
b. Pengine, hatuna uwezo wa kununua ala za muziki.

3. Ala za muziki si miongoni mwa masuala yenye manufaa (expediency), bali ni mambo yanayogusa kanuni na taratibu (linga. 1 Kor.6:12).

4. Kanisa halifanyi mambo ambayo hulifurahisha, ama kufuata hekima za kibinadamu, bali kwa huzingatia mamlaka yatokayo juu (linga. Lk.20:1-8).

5. Je, Kristo ameamuru tutumie ala za muziki ibadani leo?
a. Tunapaswa kutambua ni wakati gani sheria inatufunga?
b. Je, maoni yana fungu gani katika ibada zetu?
c. Ni mambo gani yanachangia uimbaji bila kuvunja amri? (linga. 1Kor.6:12).

6. Kanisa la Kristo limefanya utafiti wa kina katika Neno la Mungu na kugundua kwamba hakuna amri, wala mfano wa Wakristo wakimwabudu Mungu huku wakitumia ala za muziki.
a. Kwa hiyo ni upotofu ambao haujatokana na mpango wa Mungu.
b. Kwa kuwa wanafunzi wengi wa Biblia wanashindwa kuthibitisha ndani ya Agano Jipya madai ya kutumia ala za muziki      ibadani, basi aidha watakimbilia Agano la Kale au kwamba hakuna mahali Mungu amesema hapendi ala za muziki, n.k.

I. SHERIA YA IMANI

A. Tunaenenda kwa imani na wala si kwa kuona (2 Kor. 5:7).
1. Tunapata imani kwa njia ya kusikia neno la Kristo (Rum.10:17; Mt.17:5).

2. Kama tutafanya jambo bila kusikia kutoka ndani ya neno la Mungu, basi kibiblia hatuenendi kwa imani.

3. Pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu (Ebr.11:6).

B. Neno imba limetajwa mara 9, ukiondoa katika ufunuo lilivyotumika kwa namna ya mfano (Mt.26:30; Mdo.16:25; Rum.15:9; 1 Kor.14:14; Efe.5:19; Kol.3:16; Ebr.2:12; 13:15; Yako.5:13).

C. Hakuna shughuli yoyote inayolenga ibada itakayokubalika mbele za Mungu kama haijaagizwa naye.

1. Ibada inayokubalika mbele za Mungu inapaswa kuwa katika roho na kweli na wala si katika mwili, roho na kweli (Yoh. 4:24).
a. Ukweli ni neno la Mungu (Yoh.17:17).
b. Roho katika fungu hili ni utu wa ndani wa binadamu.

2. Tunapaswa kutofautisha huduma (service) na ibada (worship) – Rum.12:1-3.

3. Si kila kitu mwanadamu afanyacho ni ibada, kama Waislam wafundishavyo.

4. Ziko ibada aina nne:
a. Ibada katika roho na kweli (Yoh. 4:24)
b. Ibada ya kutungwa na wanadamu (Mt.15:8,9).
c. Ibada ya kujitungia (will-worship) – Kol.2:23. Matakwa ya mtu binafsi “arbitrary or self-devised worship.”
d. Ibada ya ujinga, huelewi mambo unayofanya ibadani (Mdo.17:22-28; Yoh.4:20-24).

D. Biblia inaagiza tunene mamoja wala pasiwepo na faraka kwa Wakristo (1Kor. 1:10).

1. Ikiwa Mungu anatuagiza kunia mamoja sisi kwa sisi na kuhitimu katika shauri moja; tukizingatia hayo ni vigumu tukatofautiana katika masuala ya msingi kabisa ya ibada (Filp.2:3-5; Rum.15:5).

2. Je, tunaweza kuwa na tumaini moja, imani moja, Bwana mmoja, Roho mmoja, ubatizo mmoja na Mungu mmoja, lakini si katika ibada moja? Efe.4:4-6.

3. Yesu aliliombea kanisa liwe na umoja, kama vile yeye alivyo na umoja na Baba (Yoh.17:20,21).

4. Watu hawajagawanyika katika masuala ambayo Yesu ameagiza, bali katika mambo ambayo hajaagiza. Hayo haswa ndiyo yanayotugawa kidini.
a. Hakuna anayepinga kuwa tunapaswa kuimba ibadani (Efe.5:19; Kol.3:16).
b. Mitume walifundisha mambo yote aliyoagiza Yesu (Mt.28:20; Yoh.16:13).
c. Roho Mtakatifu aliwaongoza mitume katika kweli yote. Ala za muziki si katika kweli yote aliyoifunua Roho Mtakatifu kwa mitume.
d. Mambo yote yafanyike kwa mamlaka ya Yesu Kristo (Kol.3:17).
i. Kuimba ni sharti kufanyike katika jina la Yesu, lakini kuimba pamoja na ala za muziki ni kinyume na mamlaka ya Yesu Kristo.
ii. Kwa kumjua (kujifunza) Kristo tumepewa mambo yote yapasayo uzima na utaua. Hatujifunzi popote Yesu na mitume wake wakitumia ala za muziki ibadani.

II. SHERIA YA IBADA
A. Kanuni za kweli za msingi kuhusu ibada ni muhimu sana kama ilivyo sheria ya imani; kwamba hakuna ibada yoyote itakayokubalika mbele za Mungu isiyoidhinishwa ndani ya Agano Jipya, Neno la Mungu.

B. Kanuni au sheria ya ibada imebainishwa katika Yoh. 4:24, “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

C. Ukweli ni nini? “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli” (Yoh. 17:17).

1. Kwa kuwa wanadamu wanapaswa kuabudu katika kweli, na neno la Mungu ndio kweli, hivyo basi, wanapaswa kuabudu kulingana na neno linavyosema.

2. Ni mahali gani ndani ya Agano Jipya panatuamuru tutumie vyombo vya muziki? Hakuna hata mahali pamoja!

3. Kuimba, ukijumuisha na ala za muziki ni kuvunja sheria ya ibada kinyume na tulivyoagizwa katika Yoh. 4:24.

III. HISTORIA

A. Ala za muziki ziliingizwa baadaye sana katika ibada kanisani (647 B.K.). Hata hivyo hazikutumika hadi kufikia karne ya nane.

1. Paul Henry Lang, “Music in Westen Civilization,” uk. 53, 54: “Vyanzo vyote vya habari vinataja uimbaji kanisani, lakini tahadhari ichukuliwe panapotajwa sanaa nyingine ya muziki… Maendeleo ya muziki Magharibi ni ushawishi uliotokana na uimbaji bila ala za muziki katika Kanisa la Kikristo.”

2. Kurt Pahlem, “Music of the World,” uk. 27: “Kuimba kwa kupokezana mistari – na neno “chant” (sio ala) limetumika, kwa karne nyingi zilizopita kabla ya ala za muziki kuingizwa katika tuni (melody).”

3. Hugo Leichtentritt, “Music, History and Ideas,” uk. 34: “Hata hivyo, kuimba tu, na si kupiga ala za muziki, kulikubalika katika kanisa la awali.”

4. Emil Nauman, “The History of Music, Juzuu 1, uk. 177: “Pasipo shaka kabisa uimbaji wa awali katika ibada takatifu kila mahali ulikuwa bila ala za muziki.”

5. Dr. Frederic Louis Ritter, “History of Music from the Christian Era to the Present, uk. 28: “Hatuna taarifa yoyote kabisa hasa ya namna ya uimbaji kanisani ulivyokuwa katika ibada za kidini katika makusanyiko ya Kikristo. Walakini, hata hivyo, tunaona kuwa ulikuwa uimbaji bila ala za muziki.”

6. Frank Landon Humphreys, “Evolution of Church Music, uk. 42: “Moja ya taswira inayotofautisha dini ya Kikristo na zingine nyingi ni utulivu wake; ilikusudia kudhibiti ishara zinazojitokeza nje kupitia hisia za ndani. Tabia zisizo za kiustaarabu, tena za dini ya Kiyunani, wakicheza na kuamasika kwa mitindo mbalimbali ili kudhihirisha hisia zao… Wakristo karne ya kwanza walijizuia kuonesha ishara za kusisimka, tangu mwanzo kabisa, muziki waliotumia, uliendana na msingi wa dini yao – utulivu wa utu wa ndani. Uimbaji uliotumika katika ibada zao awali kabisa ulikuwa ni kuimba bila ala za muziki.”

7. George Park Fisher, “History of the Christian Church, uk. 65, 121: “Awali kabisa uimbaji kanisani sehemu kubwa ulihusisha kuimba Zaburi, ukistawi haswa sehemu za Shamu (Syria) na Alexandria. Uimbaji ulikuwa wa kawaida kabisa. Palikuwa na aina nyingine za uimbaji katika ibada ya Wakristo, kama inavyoelezwa na Pliny. Katika Antiokia walianzisha uimbaji wakitumia ala (antiphony), mhusika ni Ignatius… Muziki wa kanisa la kwanza kabisa ulikuwa wa kwaya ukijumuisha kusanyiko zima.”

8. John Kurts, “Church History, Juzuu 1, uk. 376: “Awali kabisa uimbaji kanisani ulikuwa wa kawaida, usio wa kisanaa, wa kughani. Lakini kuibuka kwa uasi kulipelekea kanisa la Orthodox litilie manani sanaa zaidi. Chrysostom alipaza sauti dhidi ya kuigia kwa muziki wa kidunia kanisani. Upinzani uliendelea ukipinga ala za muziki kujumuisha katika uimbaji.”

9. Joseph Bingham, “Works,” London Edition, Vol, II, uk. 482-884: “Muziki kanisani ni wa zamani kama vile walivyo mitume, lakini ala za muziki si hivyo… Matumizi ya ala za muziki, hakika, ni suala la hivi karibuni, na si katika ibada za kanisa… Eneo la Magharibu, ala hazikutambulikana hadi karne ya nane; maana kinanda cha kwanza kuonekana Ufaransa kilipelekwa na Kostatino Kopronymus, mfalme wa Uyunani kama zawadi kwa Mfalme Pepin… Lakini, kilitumika ukumbini kwa binti wa mfalme tu, hakikuingizwa kanisani; wala ala za muziki hazikupokelewa kabisa katika makanisa ya Uyunani, hazitajwi mahali popote katika Liturugia, aidha la kale au hata la sasa.

10. Edward Dickinson, “Music in the History of the Western Church,” uk. 55: “Mtakatifu Ambrose anaonesha kuwadharau watu wanaopiga kinubi na zeze badala ya kuimba tenzi za rohoni na zaburi; na Mtakatifu Augustine anawataka waumini wasikengeuke mioyoni mwao kwa kufuata ala za muziki. Miongozo ya kidini kwa Wakristo wa awali haikukubaliana na hilo (incongruity), na hata kuona ni kufuru, kutumia vitu ambavyo huamsha ashiki, matokeo ya ala za muziki kwa mambo yasiyoonekana, ibada ya kiroho. Shauku yao kuu kidini na kimaadili si kuongeza vichocheo vya nje; uimbaji bila ala ulikuwa ndio njia pekee ya kuelezea imani yao.”

B. Psallo na Psalmos

1. Kuna watu wanaojaribu kutetea matumizi ya ala za muziki ibadani kwa kutaja neno “psallo,” kwamba maana ya neno hili linauhusiano na ala za muziki.

2. Neno “psallo” limetokea mara tano katika Agano Jipya (Rum.15:9; 1 Kor.14:15 (mara mbili hapo); Efe.5:19; Yak.5:13, bila kuwa na maana tofauti kabisa, tafsiri (versions) zote zinazokubalika – King James, English Revised, American Standard, na Douay (Roman Catholic) – hulitafsiri neno “psallo” kuwa “imba, imba zaburi, imba sifa, lahani au tuni (melody).”

a. Hakuna hata tafsiri moja inayotafsiri kuwa ni kupiga ala za muziki.

b. Hata tafsiri maarufu za kisasa za siku hizi (Goodspeed, Weymouth, Moffat, na Knox) zote zinatafsiri “psallo” kimsingi sawa na hizo tafsiri zinazokubalika.

c. Watu waliotoa tafsiri hizo zote ni miongoni mwa watu waliobobea kitaaluma katika lugha ya Kiyunani, wangetafsiri kuwa ni ala kama ingemaanisha hivyo.

3. Moulton na Milligan, walioandika moja ya kamusi zinazotegemewa na kuaminiwa, wakishughulikia Kiyunani cha Agano Jipya, hulitafsiri neno “psallo” kama lilivyotumika katika Agano Jipya: kuimba tenzi za rohoni.”

4. Abbott-Smith anachangia akithibitisha maana iyo hiyo: “…katika A.J. kuimba tenzi za rohoni, kuimba sifa.” Uthabiti wa maelezo ni wa kweli tunapoangalia mazingira yaliyotumika ya “psallo” na waandishi wa A. J; maana mjadala si juu ya matumizi ya neno, bali lilimaanisha nini kwa waandishi walioandika Agano Jipya.

5. Matumizi ya neno katika Yakobo 5:13 ni mfano dhahiri kuonesha kwamba waandishi wa Agano Jipya hawakuwaza kabisa akilini mwao suala la ala za muziki kwa neno hilo: “ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi [psallo].” Kuimba, muziki bila ala za muziki, ni namna ya kudhihirisha furaha na shamrashamra, jambo ambalo wanadamu wanao uwezo wa kufanya hivyo katika maisha ya kila siku.

a. Kama neno “psallo” lilivyotumika katika Yakobo lingemaanisha ala za muziki, basi ili mtu mwenye moyo wa kuchangamka atii ingemlazimu kutafuta ala za muziki bila kujali yuko wapi – kazini, michezoni, nyumbani au akiwa safarini.

b. Maneno (Efe.5:19) “kumshangilia Bwana mioyoni mwenu” – Kiyunani “psallontes” kutoka neno “psallo.”

c. Katika Kol.3:16, “huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu ni sawa na “kumshangilia Bwana mioyoni mwenu.”

d. Nomino inaoungana na “psallo” ni “psalmos” iliyotafsiriwa kuwa zaburi katika Agano Jipya.

e. Dr. Marvin R. Vincent, akiandika katika “World Studies of the New Testament, uk. 506, anatoa maoni yafuatayo kuhusu matumizi ya neno zaburi katika Agano Jipya: “Zaburi asilia ziliimbwa zikiambatana na ala za muziki za nyuzi. Dhana ya kujumuisha ala za muziki ikapitwan na wakati, kisha kutajwa kwa neno zaburi katika Agano Jipya ni zaburi za Agano la Kale au utenzi wenye sifa hizo.”

f. Bagster anasema hivi kuhusu “psalmos,” “nyimbo takatifu, zaburi, 1 Kor.14:26; Efe.5:19;” n.k.

g. Mfano mwingine wa matumizi ya neno “psalmos” ni katika Luka 20:42, “Maana, Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi…” Kama waandishi wangemaanisha “psalmos” kuwa ala za muziki, basi ingetafsiriwa hivi: “Maana, Daudi mwenyewe katika chuo cha kupiga ala za muziki, au chuo cha zaburi kutafsiriwa kwa kujumuishwa na ala za muziki. Kufikiri hivyo ni upuuzi!”

i) Kanisa la awali lilikuwa likifahamu vema Kiyunani na lilitumia lugha ya Kiyunani (hata Agano Jipya liliandikwa katika lugha hiyo), hawakuona vema neno “plasmos” na “psallo” kutafsiriwa kuwa ala za muziki.

ii) Wasomi walioandika kamusi za Kiyunani hawajatafsiri maneno “psalmos” na “psallo” kuwa ni kupinga ala za muziki.

iii) Waliotoa tafsiri (versions) maarufu pamoja na hizo zinazopendwa sana za kisasa, hawajatafsiri maneno “psalmos” na “psallo” kuwa ni ala za muziki.

iv) Kama maneno hayo yangemaanisha kupiga ala za muziki, basi kila Mkristo angepaswa kupiga ala za muziki kulingana na Efe.5;19 “Mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu.” Na katika Kol.3;16, “Mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni…”

IV. SABABU WATOAZO KUTUMIA ALA ZA MUZIKI

A. Hudai Agano jipya halisema ni makosa kutumia ala za muziki.
1. Katika chakula cha Bwana tumeamuriwa mkate usiotiwa chachu na mzao wa mzabibu. Je, ni sahihi kutumia nyama na viazi kwa sababu Bwana hajasema msitumie nyama na viazi mahali popote katika Agano Jipya?

2. Mungu alipowaambia Walawi wachukue moto madhahabuni kwa ajili ya kufukizia uvumba hekaluni, kwa kutaja hivyo alizuia moto mwingine wowote kutoka mahali popote pale (Law.10:1-2; 16:11,12).

3. Mungu ameagiza katika Agano Jipya tuimbe, mambo aliyonyamaza si ruhusa kwetu kabisa kuyafanya.

4. Kufundisha mambo ya Agano ya Kale ni kinyume na jinsi mitume walivyoamuriwa kufundisha, “Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi [mitume] hatukuwaagiza” (Mdo.15:24). Lazima tuheshimu Maandiko yanaponyamaza.

B. Watu hudai kwamba kwa kuwa Agano la Kale walitumia ala za muziki kwa nini leo tusitumie?
1. Yesu aliigongomelea torati msalabani na kuifuta isiwepo tena (Kol.2:14).
2. Leo, kanisa halimsikilizi Musa, bali Kristo (Yoh.1:17; Mt.17:5; 28:18).
3. Agano Jipya ni bora kuliko Agano la Kale (Ebr.8:6).
4. Ikiwa mtu anapenda kutumia vyombo vya muziki, basi inampasa kushika torati yote (Gal.3:10; Kumb.27:26; Law.18:5, n.k.).

C. Madai mengine ni suala la kuchangia tu uimbaji!
1. Wanaotoa madai haya hushindwa kutofautisha maneno kuchangia na kuongeza katika maagizo ya Mungu.

2. Neno mbao ni la jumla/ainasafu (generic). Kuna majina ya kipekee mengi kutoka ainasafu hiyo yanayobainisha mbao, kwa mfano mninga, mvule, msonobari, n.k.

3. Mwanzo 6:14, Nuhu aliambiwa atumie mvinje; kwa kuwa miti ni mingi duniani, unadhani angempendeza Mungu angetumia mti wa mninga, msonobari, mvule, n.k.?

4. Nuhu alifanya kila jambo aliloamuriwa na Mungu kikamilifu (linga. Mwa.6:22). Angetumia mti mwingine asingekuwa amechangia katika amri ya Mungu, bali angeongeza.

5. Mungu ametuagiza kuimba, unadhani atapendezwa tukiongeza kucheza, kupiga makofi, kupiga ngoma, gitaa, zeze, vinubi, n.k.?

6. Mungu hapendi wakati wote wanadamu waongeze wala kupunguza katika sheria zake (Kumb.4:2; 12:32; Mith.30:5,6; Ufu.22:18,19; 1 Kor.4:6).

7. Neno muziki ni neno la jumla/ainasafu. Kama Mungu angesema katika Agano Jipya pigeni muzika katika ibada, tungekuwa na uchaguzi: (1) muziki wa ala (2) sauti za vinywa vyetu, au (3) ala za muziki zikiambatana na sauti za binadamu.

8. Vitu vifaavyo, visivyo haribu amri ya kuimba ni: vitabu vya nyimbo, uma wa tuni (pitch pipe), kupanga sauti, pamoja na vyote visivyovunja amri ya kuimba.

9. Ala za muziki huwakilisha tendo lingine katika uimbaji tofauti kabisa na kutumia vitabu vya nyimbo, maiki, spika, n.k.

10. Mnyama ni neno la jumla/ainasafu (generic). Kuna wanyama wengi katika ainasafu hiyo kama vile: farasi, ng’ombe, kondoo, n.k.

a) Katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, Mungu aliwaagiza mnyama wa kutoa – mwana kondoo (Kut. 12:5).

b) Je, wasingevunja sheria kama wangetumia mnyama mwingine?

c) Au, ingekuwaje kama wangechinja mwanakondoo wakati wa Pasaka pamoja na wanyama wengine wasioagizwa?

11. “Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze” (Kumb. 12:32).

D. Wengine hudai kuna ala za muziki mbinguni, kama alivyoona Yohana (Ufu.5:8; 14:1,2; 15:2).
1. Iwapo tutachukulia “wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne … kila mmoja wao ana kinubi…” (5:8), kuwa ni lugha nyepesi ya kawaida, basi tunapaswa kutafsiri kuwa vitu halisi: wenye uhai wanne, wazee ishirini na wanne, sauti ya radi, vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, mwanakondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto!” (neno ‘kama’ huashiria tashibiha) – “kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu, … kama sauti ya wapiga vinanda (14:2).

2. Suala hilo lingekuwa ni sahihi, basi tungengojea kufika mbinguni na kushuhudia ala hizo Mungu alizoziweka huko. Hapa mada yetu ni jinsi gani tumeagizwa kuimba kanisani! Kuna uhusiano gani mambo ya mbinguni na yale tuliyoagizwa hivi sasa kanisani?

E. Wengine hudai ala za muziki tunazofurahia majumbani kwa nini tusifurahie kanisani?
1. Kuna mambo mengi ambayo ni halali kufanyika majumbani, lakini hayawezi kufanywa ibadani; k.m. kuosha mikono, kula chakula, kuangalia Runinga, burudani mbalimbali, n.k.

2. Je, tuingize masuala ya majumbani mwetu katika ibada kwa Mungu? (linga. Kumb.12:13, 15).

F. Wengine hudai, makusanyiko yana watu wenye vipaji vya kupiga ala za Muziki, kwa nini tusiwatumie?
1. Vipi kuhusu wapishi wazuri wa keki watuandalie keki kwa ajili ya chakula cha Bwana?

2. Unaonaje kuhusu vijana wenye vipaji vya kuchekesha tuwatumie ibadani, watuburudishe badala ya kusikiliza mafundisho ya Biblia?

Mwapotea Kwa Kuwa Hayajui Maandiko

Sheria yako naipenda mno ajabu, ndiyo kutafakari kwangu mchana na usiku. Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga” Zaburi 119:97, 130

Wakristo walio wengi wanatambua jinsi Mungu alivyofanya kazi kwa takribani miaka 1,500, na waandishi 40 tofauti tofauti ili kutupa Neno lake takatifu. Neno lililotolewa ili kufunua mapenzi ya Mungu kwa wanadamu (Yohana 5:28:11-13). Nasi vivyo hivyo tunatambua kwamba tukishabatizwa, ni lazima tufundishwe kuyashika yote, Mathayo 28:20. Tunatakiwa kuyatamani maziwa yasiyoghoshiwa ya Neno la Mungu, Petro 2:2. tulishike lililo jema, 1 Wathesalonike 5:21. Kulitumia kwa halali neno la kweli, 2 Timotheo 2:15.  Tuachane na maziwa na tuufikie utimilifu, Waebrania 6:1,  wakati huo huo tunaendelea kuwafundisha wengine kuyashika tuliyojifunza., 2 Timotheo 2:2.

Tumebarikiwa mno kuwa na maneno haya yakiwa yameandikwa kwenye kurasa, 2 Timotheo 3:16-17. Maneno ambayo kwayo twaweza kujifunza hasa Mungu anachotaka tujue, kufanya na kutii ili tuwekwe huru, Yohana 8:32; Waebrania 5:9.

Licha ya kuwa na ukwasi kama huu duniani, ni fedheha bado ipo njaa ya kulazimisha au ya kujitakia. Sio njaa ya ngano au mkate, bali njaa ya neno la Mungu kama vile alivyotangaza nabii Amosi, Amosi 8:11. Na sio kwamba maneno ya Mungu hayapo, ni kwamba leo wengi wamejisababishia njaa ya kiroho maishani na majumbani mwao kwa visingizio, kuridhika, ajizi, uvivu, n.k. licha ya kuificha injili kwa waliopotea (2 Wakorintho 4:3); twafanya vema kujificha injili.

Yaweza kusemwaje  juu ya wale ambao hawasomi tena neno la Mungu? Tayari wanafahamu kuwa ni kitabu bora kupata kuandikwa.Ndani yake kuna hadithi ya upendo iliyopata kusimuliwa. Na jinsi ambavyo ndani yake yamo maneno yaongozayo kwenda kwenye uzima wa milele. Bado kwa wengi, kiwango fulani cha kumfahamu Kristo na kanisa kinatosha kuwafurahisha.  shauku na ghamu ambayo wanapaswa kuwa nayo, ilishatoweka zamani.

Nataka tuangalie kwa haraka Mathayo 22:29-32. Twaweza kuona hapa Yesu na Masadukayo walikuwa wanazungumizia juu uhalisia wa ufufuo. “Yesu akajibu akawaambia, Mwapotea kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu,” Mathayo 22:29. Maana ya Yesu ni dhahiri, Masadukayo walishikilia imani potofu juu ya fundisho hili, kwa sababu walishindwa kuyasoma maandiko. Jibu lilikuwepo, na walichotakiwa kufanya ni kusoma na kujionea wenyewe. Bado hawakuweza kwa sababu fulani fulani.

Kuna namna kadha wa kadha inayoweza kutumika kuwianisha mistari hii na hali ya leo. Ninachotaka tujikite nacho ni kwamba tunatakiwa kujifunza kwamba Mungu “ametukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa,” 2 Petro 1:3. Na kama tukikataa kujifunza maandiko, na kuijua kweli kuhusiana na mafundisho fulani, ndipo tunakuwa na hatia kama Masadukayo vile vile, kama Yesu alivyosema, “Mwapotea.”

Unaweza kudhani kuwa, kwa hiyo “napotea” kidogo kwa kutojua fundisho la Kristo kama inipasavyo. Na upungufu huu wa ufahamu unaweza usikunyime usingizi. Walakini ilipasa ukunyime usingizi. Maana, katika Mathayo 22:29 Yesu aliposema “mwapotea kwa kuwa hamyajui maandiko.” Yesu aliwajulisha Masadukayo kuwa huu “haukuwa ufinyu wa uelewa.” Huu ni ukosefu unaoumiza ambapo wautendao watahukumiwa kwa huo.”

Tuzingatie kuwa utohoaji wa neno “kosea” katika Kiyunani ni “planao,” neno ambalo limetokana na neno la Kiyunani “plane.” Humaanisha “sababisha kukosea, tangatanga, potea,potosha, hangaika na kuwa nje ya njia.” Hivyo, hapa tunaona Yesu alivyowachukulia  ambao hawakuyajua maandiko kama iwapasavyo, ingawaje walikuwa na fursa kufanya hivyo. Walikuwa wanapotea tu!

Bado hata sasa ningali sifahamu endapo kuna watu  watakaokuwa wanafahamu nguvu ya maneno “Planao” na “plane.” Labda tukiangalia mahali pengine ambapo maneno hayo yametumika inaweza kutusaidia kuelewa kiuhalisia jinsi alivyowachukulia walioshindwa kupenda na kujua maandiko kama walivyopaswa. Hebu tuone aya mbili:

    1. 2 Wathessalonike 2:3, 11 Mtu yeyote asiwadanganye kwa njia yoyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;
    2. Neno “nguvu” katika mstari wa 11 limetokana na neno “plane” ambalo tumetoka kuliona. Ona katika mstari wa 3, Paulo aliwaonya ya kwamba mtu yeyote asiwadanganye. Na katika mstari wa 10, Paulo anabainisha kwamba wale wasioipenda kweli ndipo katika mstari wa 11, wataletewa nguvu (plane), na watauamini uongo kabisa. Na madhara ya kuuamini uongo huu yapo katika mstari wa 12, HUKUMU!
  • Warumi 1:27-wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyowapasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.Unajua  neno “potea” liko kwenye kiyunani? Uko sahihi, kama lililopo hapo juu, “plane.”

Hivyo, twaweza kuona matumizi ya aina mbili ya neno lile lile alilolitumia Yesu alipowashutumu Masadukayo kwa kutojua maandiko kama walivyopaswa. Matumizi ya kwanza huonyesha kuamini mafundisho ya uongo, ambapo huleteleza hukumu ya adhabu. Na matumizi ya pili huhusisha ushoga, ambapo pia hupelekea hukumu ya adhabu.

Tuzisome Biblia zetu kama itupasavyo! Tusibweteke na machache tunayoyafahamu! Bali kama vile kurungu avalishwavyo kwa maji, nasi tuyavae Maneno ya ajabu ya Uzima!

‘KUAMINI’ MAANA YAKE NINI?

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu,hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe nauzima wa milele” Yohana 3:16. Mstari huu ni moja ya mistari inayopendwa katika Biblia, na bado ni moja ya mistari ya Biblia iliyokosewa kueleweka. Sintofahamu hiyo hutokana na watu kuchanganya maana ya “kuamini”. Wengine hufundisha kuwa neno “amini” hapa humaanisha tu kumtambua Yesu kama mwokozi, na kwamba endapo wakifanya hivyo wanakuwa kwenye hali ya kuokolewa.

Neno “amini” katika Yohana 3:16 hutokana na neno la Kiyunani pisteuo, linalomaanisha ushawishi, tumaini la furaha, muunganiko wa utiifu. Neno “amini” katika Agano Jipya mara nyingi hubeba dhana ya utii. Neno hili pekee yake halimaanishi “saini ya kifikra.”

Mtu anaweza kutazama mazingira ambayo waziwazi Yohana 3:16 huangukia na ataweza kuona ushahidi kwamba katika mstari huu Yesu alimaanisha mambo mengi zaidi ya saini ya kifikra.  Mazingira yenyewe ni Yohana 3:1-21. Na katika mistari hii twajifunza mambo matatu ambayo nataka kuyazingatia:

  1. Ili mtu awe ndani ya Yesu, ni lazima azaliwe mara ya pili, kuzaliwa kwa maji na kwa roho, Yohana 3:1-8.
  2. Katika Yohana 3:14 kuna nukuu ya Musa kumwinua nyoka jangwani. Hata kale, waliomtenda Mungu dhambi, hawakukaa tu nyumbani huku wakiamini kuwa yule nyoka wa shaba angewaokoa. Kimsingi walitakiwa kuinuka, kutembea kutoka hemani mwao, ambapo yawezekana ilikuwa ni umbali wa maili kadhaa (kumbuka kulikuwa na kambi ya watu wapatao milioni tatu) ili kufika mahali palipokuwa na yoka wa shaba ili kumtazama ili wawe hai, Hesabu 21:9. Ni wazi kwamba katika wokovu wao kulikuwa na zaidi ya saini ya kifikra

3) Yesu alidhihirisha kwamba endapo unataka kuijia nuru, kulikuwa na jambo ambalo mtu ulitakiwa kulifanya, “Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru,” Yohana 3:21.

Tuelewe kutokana na Neno la Mungu kuwa imani ya Kibiblia huhusisha imani inayompelekea mtu kutumaini na kutii. Kushindwa kutumaini na kumtii Yesu ni kushindwa dhahiri kumpokea kama Bwana na mwokozi. “Na kwanini mwaniita Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?” Luka 6:46

Tafadhali Ukubali Kujulishwa Habari Ya Kanisa la Kristo

TAFADHALI UKUBALI KUJULISHWA HABARI YA KANISA LA KRISTO

Na Dale Dennis

Tunakujia wewe, katika jina la Kristo tu, tukiwa na hamu ya kukusaidia katika kutafta njia ya kweli ya uzima na tukitumaini kukusaidia katika kila jambo lililo haki.

Tunaamini kuwa Biblia ni andiko lenye pumzi ya Mungu ambalo linakamilisha watu na, kwa hiyo, Biblia PEKE YAKE ndiyo fundisho letu (2 Tim. 3:16-17).

Tunaomba kwa ajili ya umoja wa wote wanaomwamini Kristo kwa kuwa ndivyo alivyoomba Kristo Mwenyewe (Yoh. 17:20-21).  Paulo aliwasihi Wakristo wawe na “nia moja na shauri moja” (1 Kor. 1:10); akanena msingi wa pekee wa umoja katika Waefeso 4:1-6.

MAMBO MENGI YAKUPASAYO KUYAJUA

Inakupasa kujua kwamba:

Kanisa lilijengwa na kununuliwa na Yesu Kristo, Mat. 16:13-18; Mdo. 20:28.

Kanisa lilijengwa juu ya Yesu aliye msingi wa pekee, 1 Kor. 3:11.

Kanisa halikujengwa juu ya Paulo, wala Apolo, wala Kefa, wala mwingine awaye yote, 1 Kor. 1:12-13; 3:5.

Kanisa lilianzishwa, likasimamishwa imara katika siku ya Pentekoste ya kwanza baada ya kufufuka kwake Kristo aktika wafu, Lk. 24:49; Mdo. 1:8; Mk. 9:1; Mdo. 2:1-47.

Inakupasa kujua kwamba Kanisa si jengo au nyumba kama wanadamu wanayojenga, bali Kanisa ni watu:

Kol. 1:18; 1 Kor. 12:12-13, 27; 3:16; 1 Pet. 2:5; Mdo. 17:24.

Inakupasa kujua kwamba, katika Agano Jipya Kanisa limeitwa:

Hekalu la Mungu – 1 Kor. 3:16.

Mwili wa Kristo – Kol. 1:24; Efe. 1:22-23.

Ufalme wa Mwana wa Mungu – Kol. 1:13.

Nyumba ya Mungu – 1 Tim. 3:15.

Kanisa – Efe. 3:10.

Kanisa la Mungu – 1 Kor. 1:2; Mdo. 20:28.

Kanisa la Wazaliwa Wa Kwanza – Ebr. 12:23.

Makanisa ya Kristo – Rum. 16:16.

Inakupasa kujua kwamba watu ambao wamezidishwa katika Kanisa na Bwana huitwa:

Viungo vya mwili wa Kristo – 1 Kor. 12:27.

Wanafunzi – Mdo. 6:1.

Walioamini – Mdo. 5:14.

Watakatifu – Mdo. 9:13.

Makuhani, Ukuhani – Ufu. 1:6; 1 Pet. 2:9.

Wana wa Mungu – 1 Yoh. 3:1-2.

Wakristo – Mdo. 11:26, 28; 1 Pet. 4:16.

Inakupasa kujua kwamba katika Kansia kuna:

Wazee ambao wote ni maaskofu (Tito 1:5-9) na waangalizi (Mdo. 20:17-18, 28) na wachungaji (1 Pet. 5:1-4).  Si kana kwamba tumetaja aina nne za watu wenye kazi mbalimbali, la sivyo!  Sura hizo zinatuaonyesha wazi kwamba kila mzee wa kanisa ni askofu, na mwangalizi na mchungaji pia; kwa kuwa, kazi yake ni kuangali, na kuchunga, na kutunza na kulisha kanisa.  Mtu hawezi kuwa mzee wa kanisa isipokuwa ametimiza yote yaliyoandikwa katika 1 Tim. 3:1-7 na Tito 1:5-9.

Katika kansia kuna mashemasi.  Kazi yao ni kulihudumia kanisa, 1 Tim. 3:8-13;  Mdo. 6:1-6.

Katika kanisa kuna kuhani mkuu.  Yesu Kristo ni kuhani mkuu wetu na hakuna mwanadamu awaye yote awezaye kuwa kuhani mkuu pamoja na Kristo, Ebr. 4:14; 7:23, 24, 28; 7:11, 12; Rum. 6:14; Gal. 3:23-26.

Katika kanisa kuna makuhani, KILA MKRISTO ni kuhani (Ufu. 1:6; 1 Pet. 2:9) na kazi ya kila Mkristo ni kujitoa mwili wake uwe “Dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu,” Rum. 12:1, na kumpa “dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliyoungama jina lake,” na sadaka ya “kutenda mema na kushirikiana” Ebr. 10:12-14; 9, 12.  Lakini, tunapokula chakula cha Bwana, si kana kwamba tunamtoa Kristo awe dhabihu tena; bali chakula cha Bwana ni ukumbushao tu wa kifo chake (1 Kor. 11:23-26).

Inakupasa kujua kwamba mwanadamu:

Hakukusudia kanisa, bali Mungu alikusudia, Efe. 3:10-11.

Mwanadamu hakununua kanisa, bali Yesu alinunua, Mdo. 20:28; Efe. 5:25.

Mwanadamu hakuwapa watu wa kanisa jina lao, bali Mungu aliwapa jina, Isa. 62:2; Mdo. 11:26.

Mwanadamu hakuliita kansia kuwa ni mali yake, bali Yesu aliliita kanisa kuwa ni lake, Mat. 16:18.

Mwanadamu si kichwa cha kanisa, bali Yesu ni kichwa cha kanisa, Efe. 5:23; 4:4; 1:22, 23.

Mwanadamu si mwokozi wa kanisa, bali Yesu ni mwokozi wake, Efe. 5:23.

Mwanadamu hakulipa kanisa mafundisho yake, bali Yesu alilipa mafundisho yake, Gal. 1:11; 2 Pet. 1:20-21; 2 Yoh. 9-11.

Mwanadamu hakulizidisha kanisa, bali Yesu alizidisha kansia kwa wale waliokolewa, Mdo. 2:47.

Inakupasa kujua kwamba kanisa na mwili wa Kristo ni mamoja:

Efe. 1:22-233; Kol. 1:18, 24.

Inakupasa kujua kwamba Agano Jipya linasema:

Kuna ufalme mmoja wa Kristo, Kol. 1:13-14.

Linasema kuna mwili mmoja wa Kristo, Efe. 1:22-23; 4:4.

Linasema kuna kansia moja tu la Krsito, Mat. 16:18; Efe. 1:22-23; 4:4; Yoh. 17:20-21.

Inakupasa kujua kwamba katika Kanisa tu tunaweza kupata:

Ukombozi, Efe. 1:7.

Msamaha wa dhambi katika kanisa tu, Kol. 1:13-14.

Kutakaswa katika kansia tu, Efe. 5:26.

Baraka zote za rohoni katika kansia tu, Efe. 1:3.

Inakupasa kujua kwamba ili uingie katika Kanisa ni lazima:

Kumwamini Kristo, Yoh. 8:24; Mdo. 16:31; Ebr. 11:6.

Ni lazima kuzitubia dhambi, Lk. 13:3; Mdo. 2:38; 3:19; 17:30.

Ni lazima kukiri imani yako katika Kristo, Mat. 10:32-33; Rum. 10:10; Mdo. 8:37-38.

Ni lazima kubatizwa, Mat. 28:19; Marko 16:16; Mdo. 2:38; 10:48; 22:16; 1 Pet. 3:21; Gal. 3:27.

Inakupasa kujua kwamba ubatizo:

Huhitaji maji, Mdo. 10:47.

Ubatizo huhitaji maji mengi, Yoh. 3:23.

Ubatizo huwafanya watu waende mahali penye maji, Mdo. 8:36; Mat. 3:5, 6;  Yoh. 3:23.

Ubatizo huwafanya watu waingie ndani ya maji, Mdo. 8:38.

Ubatizo humfanya mtu kuzikwa ndani ya maji, Rum. 6:3-5; Kol. 2:12.

Ubatizo humfanya mtu kuzaliwa tena, Yoh. 3:5.

Ubatizo humfanya mtu kufufuka kutoka maji, Kol. 2:12.

Ubatizo huwafanya watu kupanda kutoka maji, Mdo. 8:39; Mat. 3:16.

Inakupasa kujua kwamba katika ubatizo:

Dhambi huoshwa, Mdo. 22:16.

Twaokolewa kutoka dhambini, 1 Pet. 3:21; Mk. 16:16.

Twapata ondoleo la dhambi, Mdo. 2:38.

Twaingia katika Kristo na twamvaa Kristo, Gal. 3:27.

Twaokolewa kutoka hukumu ya adhabu, Gal. 3:27; Rum. 8:1.

Twaingia katika kanisa, Mdo. 2:27-47.

Twaanza kutembea katika upya wa uzima, Rum. 6:3-5.

Twamtii Kristo, Mdo. 10:48; Mk. 16:16.

Twapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, Mdo. 2:38; 5:32.

Inakupasa kujua kwamba ni lazima kuwa kanisa kumwabudu Mungu:

Katika roho na kweli, Yoh. 4:23-24; Rum. 12:1.

Twaabudu KILA SIKU bila kukoma, kwa njia ya kutoa miili yetu iwe “Dhabihu iliyo hai.”  Rum. 12:1.

Twaabudu katika kila neno na kila tendo, Kol. 3:17, 23, 24.

Twaabudu katika matendo mema, Efe. 2:10; Mat. 5:16; Ebr. 13:16; Mat. 25:31-46.

Twaabudu katika kuliungama jina lake Yesu “daima”, Ebr. 13:15; Mat. 10:32-33.  Hii ina maanda ya kuwa ni lazima kwa kila Mkristo kumkiri Yesu na kuifundisha Injili yake kwa watu wengine, Ebr. 5:12; Mat. 28:18-20; 1 Pet. 3:15.

Twabudu katika kuomba, Mdo. 2:42; 1 Tim. 2:1-2.

Twaabudu katika kuimba, Efe. 5:19; Kol. 3:16.

Twaabudu katika kujengana, 1 Kor. 14:26-27.

Twaabudu kwa kula chakula cha Bwana katika Siku ya Kwanza ya juma, Mdo. 20:7; 1 Kor.11:23-32; Ebr. 10:26.

Twaabudu katika kutoa changizo, 1 Kor. 16:1-2; 2 Kor. 8:1-15; 9:1-15; Mdo. 20:35.

Twaabudu kwa kudumu katika kujifunza maneno ya Mungu, Ebr. 5:12-14; 1 Pet. 2:2; Mat. 4:4.

Inakupasa kujua kwamba kazi ya kila Mkristo ni:

Kuihubiri Injili, Mk. 16:15; Mat. 28:18-20; 1 Tim. 4:1-7.

Kila Mkristo na afundishe wengine, Ebr. 5:12; 1 Pet. 2:9; 3:15; Efe. 3:10-11.

Wakristo wote wapendane na kufanya matendo mema, 1 Yoh. 3:11-18; Mat. 25:31-46; Ebr. 13:15; Efe. 2:20; Yak. 1:27; Rum. 12:1-2.

Kanisa La Baptist

Tovuti hii ni mpya ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kuwahubiria waliopotea injili isiyo ya bandia. Katika siku za usoni tutakuwa na masomo ambayo yatawajia hapa. Lakini kwa sasa, hebu niulize swali moja rahisi.Katika Mathayo 16:18, Yesu aliposema “juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu.” Ni mahali gani katika Agano Jipya alipoita kanisa “kanisa la Baptist”? Kama kanisa ni lake, sasa kwa nini kuliita kwa jina la tendo la wokovu? Tendo ambalo wabaptist wengi hawaamini kuanza nalo? Yesu alisema waziwazi ni “kanisa lake”. Ni dhahiri kwamba alilinunua kanisa kwa damu yake mwenyewe. Nasi tunaona majina ya kanisa katika Agano Jipya dhahiri shahiri. Walakini, hakuna mahali katika maandiko kwamba kanisa alilolinunua Kristo likaitwa Baptist. Hakuna. Kibiblia, mamlaka yako iko wapi ya kukufanya uliite kanisa alilolijenga Yesu, “Kanisa la Baptist”? Jina hili limetoka kwa Mungu au kwa mwanandamu? Na kama huwezi kupata mamlaka ya kibiblia ya jina la kanisa unalotumia. Je, hiyo haimaanishi kwamba basi tu huamini kwamba mamlaka ya Mungu imo katika Biblia?

Naomba ni nikuhabarishe kuhusu kanisa la Kristo. Hupatikana katika Afrika Mashariki, na ulimwenguni. Nao ni kundi la waamini, ambao sio tu wanajua kuwa Yesu alilijenga kanisa (Mathayo 16:18), Alilinua kwa damu yake mwenyewe (Mdo 20:28), bali pia ni kichwa cha kanisa (Wakol. 1:18). Hatuoni haya kuliita kanisa kwa jina la mwokozi wetu. Na wala hatuoni haya kuliita kanisa kwa jina lililoruhusiwa katika maandiko. Kwa nini Baptist wanakataa kujiita kwa jina la yeye aliyekufa kwa ajili ya kanisa lake?

Ndiyo kwanza natengeza hii tovuti kwa sasa na ni lazima nianzie mahali fulani. Vivile tunatoa masomo ya Biblia kwa masafa. Unaweza kutuma barua pepe kwenda kanisalakristo@yahoo.com ili kuomba masoma haya. Tafadhari usisahau kuandika jina na anwani yako ya posta.