Yesu alisema, “Lakini saa inakuja, nayo saa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika Roho na Kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho nao wamwabuduo Yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na Kweli,” Yn. 4:23, 24. Vitu viwili vinahitajika kwa kumwabudu kama tunataka ibada zetu zikubaliwe na Mungu.
- Ni lazima tuabudu katika roho.
Hiyo maana yake mioyo yetu lazima iwe katika hali ya haki. Ni lazima tuwe tunafikiria tukifanyacho. Isa. 1:11-20; Mith. 28:9; Mt. 15:8.
Ni lazima tumwabudu Mungu katika kweli. Kumwabudu Mungu katika kweli maana yake ni lazima kumwabudu Mungu kulingana (kufuatana) na kweli. Neno la Mungu ndiyo kweli (Yn. 17:17). Kwa hiyo, ili kuabudu kwetu kukubaliwe na Mungu, lazima kufanyike kwa kufuata neno lake.
Agano Jipya linatoa matendo ya ibada ambayo wakristo wanapaswa kuyafanya. Matendo ya ibada yaliyotolewa katika Agano la Kale kama kucheza, vyombo vya kufukiza uvumba, iliamriwa kwa taifa la Israeli tu. Agano la Kale kama sheria inayofunga kwa watu wa Mungu iliishia msalabani (Kol. 2:13, 14). Wakristo ni lazima wajifunze kutoka katika Agano Jipya, sheria ya Kristo kwa watu wote leo, jinsi Mungu anavyotaka aabudiwe leo. Matendo ya ibada yanayotakiwa na Mungu yameelezwa na kuwekwa wazi ndani ya Agano Jipya.
Chakula cha Bwana:
Chakula cha Bwana au ushirika (1 Kor. 10:16), kinajumuisha vitu viwili (1) mkate usiotiwa chachu (bila chachu) na (2) uzao wa mzabibu (maji ya zabibu). Kusudi la Chakula cha Bwana ni kuleta kumbukumbu ya dhabihu ya mwili na damu ya Yesu msalabani (Mt. 26:26-29). Ni lazima tuwe waangalifu tunaposhiriki ushirika huo kuona kuwa tunapambanua ipasavyo na kutambua damu na mwili wa Yesu ili kushiriki katika tabia inayostahili (1 Kor. 11:23-30). Wakristo ni wajibu wale Chakula cha Bwana kila Siku ya Kwanza ya kila juma (Mdo. 20:7).
Sala (Maombi):
Maombi yanayotolewa kwa Mungu yanapaswa yawe sehemu ya ibada ya jumla (au hadhara) na pia ile ya faragha au pekee. Kuna mifano mingi ihusuyo mwongozo wa mambo ya sala katika Agano Jipya (1 Tim. 2:1, 2, 8); (Flp. 4:6) n.k. Katika sala zetu kwa Mungu tunatoa shukurani zetu na kulitukuza jina lake. Katka sala zetu tunaweza kuomba kwa ajili ya mahitaji yetu na ya wengine.
Yesu alituonyesha “kielelezo” cha maombi katika Mt. 6:5-15. Hakukusudia tuwe tunairudia kama wimbo usio na maana katika mawazo lakini aliitoa kama mfano ili kuona jinsi tunavyoweza kuweka maombi yetu. Yesu Kristo ni Mpatanishi wetu na Kuhani Mkuu. Kwa hiyo sala zetu ni lazima zielekezwe kwa Mungu kwa njia ya jina la Yesu (Yn. 16:23; 1 Tim. 2:5; Ebr. 4:14-16; 1 Yoh. 2:1, 2).
Kuhubiri na Kufundisha Neno la Mungu:
Mungu ametuamuru kufundisha neno lake (Mt. 28:19,20). Wote waliookolewa na wenye dhambi wanahitaji kufundishwa. Kwa hiyo, somo toka ndani ya BIBLIA NI moja ya matendo ya ibada ambayo kwayo wakristo wanapaswa kujishughulisha (Mdo. 2:42). Ni lazima tujifunze Neno la Mungu ili tuweze kuimarika katika Kristo, kuwafundisha wengine na kuzuia mafundisho mapotofu (1 Pet. 2:1, 2; 2 Tim. 2:2; 4:1-5). Hii ni sehemu muhimu sana ya ibada yetu na kamwe tusiipuuze.
Kutoa:
Kutoa katika tulivyonavyo ni sehemu ya ibada kwa Mungu. Hii ni njia inayolifanya Kanisa la Kristo lipate fedha ya lazima kufanyia kazi yake. Mungu ametupatia mpango mkalilifu unaohusu kutoa (1 Kor. 16:2). Tumeambiwa ni nani atoe. “Kila mtu kwenu” tumeambiwa lini tutoe, “Siku ya Kwanza ya juma” tumeambiwa tutoe kiasi gani, “Kwa kadiri ya kufanikiwa kwetu.” Tunaonyesha upendo wetu kwa Mungu tutoapo kwa furaha na hiari kwake, 2 Kor. 9:7.
Kuimba:
Wakristo tumeambiwa (tumeamriwa) kumtukuza Mungu katika nyimbo (Kol. 3:16) aina ya muziki ambao Mungu ameamuru kwa ajili ya Kanisa lake ni wa mdomo tu. Huo ni kuimba. Hakuna mahali po pote penye amri au mfano katika Agano Jipya kuhusu kutumia vyombo vya muziki katika ibada ya kikristo. Kuongeza vyombo vya muziki katika kuimba kwetu ni dhambi.
Kwa sababu ya kuongeza juu ya lile ambalo mungu ametuambia analihitaji (analolitaka) hakuna mtu mwenye haki kufanya hilo (Ufu. 22:18.19; 2 Yoh. 9-11). Tunatakiwa “kushangilia ndani ya mioyo yetu” (Efe. 5:19) vyombo viwe ni vile vilivyofanywa na Mungu (mdomo) na sio watu!
Wala Mungu hajatuamuru kuwa na waimbaji maalum katika ibada yetu kama wanakwaya; kila Mkristo ni lazima amtukuze Mungu katika wimbo kama vile kila mmoja anavyoshiriki Chakula cha Bwana yeye mwenyewe. Lengo la kumwabudu Mungu sio kujitumbuiza sisi kwa sisi. Kwa hiyo, tufanyacho katika ibada siyo kile kinachovutia viungo vyetu vya ufahamu, bali lazima kiwe ni kile kimpendezacho Mungu.
Wakristo wa kweli wanataka kumwabudu Mungu. Kwa kweli haiwezekani kwa Mkristo wa kweli kutomwabudu Mungu. Tunapofahamu ukuu wa Mungu, utukufu wake, enzi yake, hekima yake na nguvu na kutafakari juu ya rehema zake zisizopimika (katika ukubwa wake) katika kumtoa mwanawe pekee ili atuokoe kutoka dhambini mwetu, mioyo yetu itafurika “matoleo (dhabihu) ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake,” (Ebr. 13:15)
Na Rod Rutherford